Pages

Ads 468x60px

Sunday, June 17, 2012

Stars yafa kiume Msumbiji, Maputo



NDOTO ya Tanzania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2013, imefutika rasmi jioni ya leo mjini Maputo, Msumbiji baada ya kukubali kufungwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 8-7 na Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto jijini hapa katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Timu hizo zilifikia hatua ya mikwaju ya penalti baada ya kumaliza dakika 90 matokeo yakiwa 1-1 kama ilivyokuwa mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam, hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa 2-2.
Msumbiji ‘Mambaz’ walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza lililofungwa na Jeremies Saito aliyeunganisha kwa umakini krosi ya Helder Pelembe dakika ya 18.

Wakati mashabiki wa Msumbiji wakiamini mchezo umeisha, beki Aggrey Morris aliisawazishia Kili Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro, akiunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Amir Maftah dakika ya 90 na kufanya kwenda kwenye changamoto ya mikwaju ya penalti.

Nahodha wa Stars, Juma Kaseja alipangua penalti mbili za kwanza za Msumbiji, kabla ya Mbwana Samata kukosa penalti ya tisa iliyopanguliwa na kipa Joas na wenyeji Mambaz kupata ya kwao iliyofungwa na Dominguez.

Waliopata penalti kwa Stars ni Amir Maftah, Shomari Kapombe, Shaaban Nditi, John Boko, Frank Domayo na Mrisho Ngasa, wakati Morris, Kelvin Yondani na Samata wakikosa.

Pamoja na kufungwa bao la mapema, Stars iliweza kutulia na kucheza soka ya kujiamini katika kipindi chote cha kwanza, lakini washambuliaji wake walikosa umakini kwenye umaliziaji.
Samata alikosa bao dakika ya 24 baada ya kupokea mpira uliomtoka beki wa Msumbiji, lakini alipiga shuti hafifu likaishia mikononi mwa kipa.

Kiungo Domayo, alionesha soka ya kiwango cha juu kwa kutoa pasi za uhakika na kuwaunganisha vema Ulimwengu na Samata mwanzoni.

Hata hivyo, Kocha Kim Poulsen, alilazimika kufanya mabadiliko ya kikosi kipindi cha pili kwa kuwatoa Ulimwengu, Mwinyi Kazimoto na Erasto Nyoni na kuwaingiza Haruna Moshi, Boko na Maftah, mabadiliko yaliyokuwa na faida kubwa kwa Stars.

Wenyeji walicheza kwa nguvu huku wakishangiliwa na mashabiki wao, lakini walishindwa kuipenya ngome ya Stars chini ya Aggrey.

Stars: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Shaabani Nditi, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samata, Mwinyi Kazimoto. 

0 comments:

Post a Comment