Nchi yetu iko njia panda. Tuna
nchi nzuri yenye bioanuai za wanyama na mimea ambazo
haziwezi kufananishwa na nchi nyingine yeyote. Takriban asilimia 40 ya eneo
lote la nchi limehifadhiwa kwa ajili ya misitu na wanyamapori. Hata hivyo,
uharibifu wa misitu unafanyika kwa kasi ya kutisha. Takriban ekari milioni moja
za misitu zinateketezwa kwa mwaka. Karibu mabonde na mifumo yote ya mito mikuu
hapa nchini inaanzia kwenye misitu ambayo sasa tunaiharibu kwa kasi ya kutisha.
Kuna mambo kadhaa
yanayochangia kasi hii kubwa ya uteketezaji wa misitu hapa nchini, ikiwemo
ufyekaji wa maeneo kwa ajili ya kilimo, mifugo, uchomaji wa mkaa na biashara ya
kuni. Hakuna shaka kwamba mahitaji ya mkaa na kuni yanazidi uwezo wa misitu
yetu ya asili kukukidhi mahitaji hayo. Mahitaji haya yataendelea kuongezeka kwa
kasi kwa miaka inayokuja kutokana na ukuaji wa miji na ongezeko la idadi ya
watu, kwani inaaminika kwamba ongezeko la asilimia moja ya ukuaji wa miji linasababisha
ongezeko la asilimia 14 la matumizi ya mkaa.
Ikizingatia
kwamba, Tanzania ni moja ya nchi zinazoongoza duniani kwa kasi ya ukuaji wa
miji, kiasi kwamba ifikapo mwaka 2027 zaidi ya nusu ya Watanzania watakuwa
wanaishi mijini, mahitaji na matumizi ya mkaa yatakuwa maradufu kuliko ilivyo
sasa. Hivyo, ni muhimu sana hatua za haraka ni muhimu zichukuliewe sasa ili
mahitaji haya ya makubwa ya mkaa yasipelekee kuangamizwa kwa misitu yetu.
Kuwa na uzalishaji endelevu
wa mkaa, au kuifanya biashara ya mkaa
isiwe na tija, au mbadala wa mkaa kuwa na faida zaidi kibiashara, ni jambo la
msingi kwa usalama wa nishati kitaifa, kwa kupunguza ukataji misitu na kulinda
huduma zitokanazo na mifumo-ikolojia nchini, ikiwemo ulinzi wa vyanzo vya maji,
utiririkaji wa maji katika mito na hivyo upatikanaji wa maji nchini.
Naamini kuwa moja ya njia za
kuokoa mazingira yetu, kulinda urithi adhimu uliomo katika Hifadhi zetu, na
kurejesha thamani ya maliasili yetu ni kwa kupunguza ukataji wa misitu kwa
ajili ya mkaa. Njia bora ya kufanya hivyo ni kwa kupunguza matumizi ya mkaa
kupitia ubunifu wa teknolojia za nishati
nafuu na zenye ufanisi zaidi na endelevu; na vyanzo nafuu vya nishati mbadala
katika ngazi ya kaya.
Lakini leo tunaweza kuanza
safari ya kuondokana kabisa na matumizi ya mkaa kupitia ubunifu katika
ujasiriamali wa nishati za kupikia - hasa ubunifu kwa upande wa uzalishaji na
usambazaji wa nishati mbadala wa mkaa, na katika kuufanya mkaa kupata ushindani
mkubwa katika soko la nishati za kupikia au ubunifu katika kufanya uzalishaji
na matumizi ya mkaa kuwa endelevu (kutoharibu mazingira). Naamini kwamba
inawezekana kabisa kuanzisha na kuendeleza mifumo mipya ya uzalishaji,
usambazaji na uuzaji wa nishati ya kupikia ambayo itapunguza kasi ya ukataji
miti na kupunguza athari kwa mazingira nchini.
Ninazindua kwa mara ya kwanza
Shindano la Kitaifa la Kutafuta Mbadala wa Mkaa. Madhumuni ya msingi ya
Shindano hili ni kuwatambua, kuwatuza, kuwawezesha na kuwaendeleza wabunifu na
wajasiriamali wanaojihusisha na mbinu na jitihada za uzalishaji, usambazaji na
matumizi ya nishati endelevu za kupikia. Natoa wito kwa wadau wote: watu
binafsi, wabunifu, makampuni binafsi, wajasiriamali, asasi za kiraia na
kijamii, taasisi zisizokuwa za Kiserikali, Taasisi za Elimu ya Juu, na Taasisi
za Utafiti, kushiriki katika changamoto hii.
Moja ya madhumuni ya
ziada ya shindano hili ni kuwaleta pamoja wadau na wabunifu wanaojishughulisha
na harakati za kutafuta na kutumia nishati mbadala wa mkaa. Kama sehemu ya
mchakato huu, na hasa baada ya shindano, kutakuwa na warsha, semina, mafunzo
ambazo zitawaleta pamoja wadau wote kuendelea kutafakari jitihada za ziada za
kupata nishati mbadala wa mkaa.
Aidha, mafanikio mengine tunayoyatarajia ni
kama yafuatayo:-
§
Kuinua uelewa juu ya suala la ukataji
miti na umaskini wa nishati kwa mapana zaidi miongoni mwa watu wa kawaida;
§
Kuvutia na kuhamasisha ujasiriamali na
uwekezaji miongoni mwa wananchi katika sekta ya nishati ya kupikia;
§
Kuwezesha kuonekana kwa mawazo na fikra
mpya za watu wengi wanaojishughulisha na kupunguza matumizi ya mkaa;
§
Kuweza kubaini makundi yanayojihusisha
na ubunifu/ufumbuzi wa nishati endelevu ya kupikia na iwapo yanaweza
kuunganishwa, kuwezeshwa au kuwekwa pamoja mnyororo wa thamani ya uzalishaji,
usambazaji, uuzaji wa rejareja / jumla wa nishati ya kupikia.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- uungano na Mazingira Mheshimiwa January Makamba akiongea na Wandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya shindano la kutafuta mbadala wa mkaa, lilioandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais |
Mshindi wa kwanza atapokea tuzo ya fedha ya shilingi Milioni Mia Tatu (300,000,000), mshindi
wa pili atapokea Shilingi Milioni Mia Mbili (200,000,000) na mshindi wa tatu
atapokea Shilingi Milioni Mia Moja (100,000,000). Zawadi hizo za fedha
zitatumika tu kwa ajili ya kukuza na kuendeleza mtaji wa miradi/ufumbuzi iliyoshinda. Vilevile, washindi hawa watatu wa kwanza watapatiwa
mafunzo ya biashara na uwekezaji kulingana na uvumbuzi wao na watatambulishwa
kwa wawekezaji na/au kupelekwa zilipo fursa zaidi za uwekezaji au ubia, ndani
na nje ya nchi, kwa ajili ya kupanua na
kuupeleka sokoni ubunifu wao. Mategemeo ni kwamba njia moja au njia zote
zilizoshinda zitakuwa zimetoa ufumbuzi wa nishati mbadala ya kupikia nchini.
Tuzo zitatolewa kupitia mchakato wa wazi
kwa tathmini mahiri ya jopo la wadau wa nishati, mazingira na wataalamu wa
biashara kwa kipindi cha miezi sita.
Kuhusu ubunifu unaohusisha
matumizi endelevu ya mkaa, masuala yafuatayo yanaweza kuangaliwa, katika kuamua
mshindi:
§ Usimamizi na matumizi
endelevu ya rasilimali za misitu na upandaji miti;
§ Teknolojia bora za
uzalishaji wa mkaa;
§ Vyanzo mbadala vya mkaa
kama vile briketi, au mkaa wa taka, nk.
§ Ubunifu katika mnyororo
wa thamani ya mkaa, na
§ Utengenezaji na
usambazaji wa majiko banifu na biashara ya mkaa.
Ubunifu/ufumbuzi utakaopokelewa kwa ajili ya kushindanishwa ni ule
ambao tayari unatekelezwa au ambao upo kwenye majaribio kwa muda usiopungua miezi
sita kuanzia tarehe ya kuwasilisha maombi ya kuingia kwenye shindano.
Andiko/pendekezo, wazo au dhana ambayo bado iko kwenye makaratasi (paper
proposal) haitafikiriwa kuingizwa kwenye shindano.
Wakati wa mchakato wa tathmini, jopo la thathmini
linaweza kutembelea maeneo ubunifu unapotumika, kuomba vifaa vinavyotumika,
kuhitaji kufanyika majaribio mara kadhaa, na kuhitaji maelezo mengine yoyote ya
ziada kwa ajili ya kufanya tathmini kamili na sahihi na ya haki.
Jinsi ya kushiriki: Waombaji
watatakiwa kujaza fomu zitakazopatikana katika Ofisi ya Makamu wa Rais, iliyopo
Mtaa wa Luthuli, jijini Dar es Salaam, au kupakuliwa kutoka tovuti ya Ofisi ya
Makamu wa Rais (www.vpo.go.tz) kuanzia
tarehe 15 Disemba 2016. Vilevile, watatakiwa kuwasilisha andiko la
ubunifu/ufumbuzi wao lenye kujibu maswali yafuatayo:-
- Je, ubunifu/ufumbuzi huu unaweza kupanuliwa (scalability) na kutekelezwa, kuzalishwa na kuigwa katika maeneo mengi nchini?
- Je, ubunifu/ufumbuzi huu utaweza kuwa endelevu na kutekelezwa kwa muda mrefu bila ukomo (sustainability)?
- Je, ubunifu/ufumbuzi huu utaweza kutekelezwa/kupatikana nchi nzima, hasa kwa watu wa kipato cha chini?
- Je, ubunifu/ufumbuzi huu utatoa unafuu wa gharama ya nishati ya kupikia kuliko mkaa?
- Je, ubunifu/ufumbuzi huu ni kwa namna gani unaweza kuwa biashara yenye faida (commercially viable) kwa mbunifu na mwekezaji?
- Je, ubunifu/ufumbuzi huu utaweza kuwa na faida gani na kwa kiasi gani kwa mazingira na kijamii?
Imani yangu ni kwamba shindano
hili litaendana na hatua nyingine za kisera za kudhibiti ukataji wa misitu,
kulinda vyanzo vya maji, kuondoa umaskini wa nishati, na kuifanya bei ya mkaa
itokane na thamani halisi ya miti iliyotumika kutengeneza mkaa huo.
Uchukuaji na urudishaji
fomu za kushirikiki kwenye shindano, pamoja na mawasilisho ya maandiko,
yatapokelewa kuanzia tarehe 15 Desemba 2016 hadi tarehe 31 Januari 2017. Tuzo
kwa washindi zitatolewa mwezi Juni 2017. Mawasilisho yanaweza kuwa kwa lugha ya
Kiingereza au Kiswahili na hakutatozwa ada kwa ajili ya fomu na mawasilisho.
Maelezo ya ziada ya
shindano hili nitayatoa tarehe 29
Novemba 2016, katika kikao cha wadau
wa mkaa nilichokiitisha siku hiyo. Katika kikao hicho pia nitatangaza
Mshirika wa Sekta Binafsi katika shindano hili.
Kwa ufanunuzi wa ziada, unaweza kuwasiliana nami
kupitia:
Facebook: Ofisi ya Makamu wa Rais
Instagram: VPOTanzania
Twitter: VPOTanzania
Simu: 0685 333 444
January Makamba (MB.)
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na
Mazingira
10 Novemba
2016
0 comments:
Post a Comment