TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UHAMASISHAJI WA KUPIGIA KURA MLIMA KILIMANJARO, BONDE LA NGORONGORO NA TUKIO LA KUHAMA WANYAMA KATIKA HIFADHI YA SERENGETI KATIKA SHINDANO LA MAAJABU SABA YA ASILI KATIKA BARA LA AFRIKA
Hivi karibuni pamekuwa na shindano jipya lijulikanalo kama Seven Natural Wonders, linaloshindanisha vivutio mbalimbali vya asili vinavyopatikana katika kila bara. Shindano hilo linaloendeshwa kwa kupiga kura kupitia tovuti ya http://sevennaturalwonders.org linashindanisha vivutio vya utalii kumi na viwili (12) katika bara la Afrika. Tanzania ni nchi pekee yenye vivutio vingi katika orodha hiyo. Vivutio vya Tanzania ni Mlima Kilimanjaro, Bonde la Ngorongoro, na hifadhi ya Serengeti. Watanzania na watu wote duniani wanahamasishwa kuvipigia kura vivutio hivyo vitatu (3).
Ili kurahisisha upigaji kura kwa vivutio vya Tanzania, Bodi ya Utalii Tanzania imewaomba waandaji wa shindano hilo kuandaa tovuti maalum ambayo ni http://sevennaturalwonders.org/tanzania/ itakayomuhitaji mpigakura kutuma barua pepe yenye kichwa cha habari “TANZANIA” inayoorodhesha vivutio hivyo vitatu (3), na vivutio vingine visivyozidi vinne (4) vilivyopo Tanzania ambavyo mpigakura anaona vinafaa viwemo katika orodha ya maajabu saba ya asili ya Tanzania, kwenda kwenye anuani hii vote@sevennaturalwonders.org. Kwa maelezo zaidi kuhusu vivutio vya utalii Tanzania tembelea www.tanzaniatourism.go.tz.
Shindano hili linaweza kuwa fursa nzuri kwa Tanzania kujitambulisha pamoja na kuitangazia dunia kuwa Mlima Kilimanjaro, ambao ni mlima mrefu kuliko yote barani Afrika; Hifadhi ya Serengeti, ambapo tukio la kuhama wanyama hutokea kila mwaka; na eneo la Ngorongoro, ambalo ni urithi wa dunia wa asili na utamaduni (natural and cultural World Heritage Site), vyote ni vivutio vilivyopo hapa kwetu Tanzania.
Vivutio vitakavyoshinda vitatangazwa na vyombo mbalimbali vya habari duniani na kupewa hadhi zaidi ya kimataifa.
Tumia fursa hii kupigia kura vivutio vyote vya Tanzania ili viweze kuwa miongoni mwa maajabu saba ya asili ya bara la Afrika.
Imetolewa na Mkurugenzi Mwendeshaji
BODI YA UTALII TANZANIA
0 comments:
Post a Comment